Thursday, 26 July 2012

ZITTO KABWE: ASEMA URAISI USITUTENGANISHE


Kizitto Noya, Dodoma
WAKATI wabunge Halima Mdee na Joshua Nassari wakikanusha kumsafishia njia ya urais Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, mwenyewe ameibuka na kusema kelele hizo ni siasa, kwani anaamini kama urais upo, utakuja tu. Zitto alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihitimisha mchango wake katika Hoja ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

“…Hivi karibuni tulikuwa na tamasha Kigoma ambalo limezua mjadala mkali kuhusu suala la urais. Mimi niseme tu kwamba hizi ni siasa na zitapita,” alisema Zitto na kuongeza: “Lakini naamini kwamba kama urais upo utakuja tu na kama haupo hautakuja. Ila napenda kuweka wazi kwamba uwezo, uzalendo na uadilifu wa kuwa Amiri Jeshi Mkuu sina shaka ninao.” Awali, Zitto alifafanua suala hilo kwa taarifa aliyoiweka kwenye mtandao akieleza kuwa, asingependa kuhusishwa na matamshi ya wabunge hao kupinga walichosema Kigoma, kwa kuwa ukweli utajulikana. “Katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Julai 2012, kulikuwa na habari yenye kusomeka 'Wabunge wamsafishia Zitto njia ya urais 2015'.

Habari hii imeleta mjadala mara baada ya kutoka na kusomwa. Mjadala umekuzwa zaidi baada ya Mdee na Nassari kukanusha maneno waliyonukuliwa kuyasema. Alisisitiza kuwa ukweli utajulikana kwa mkanda wa video uliorekodiwa kwenye hafla hiyo atakaouweka kwenye blogu yake hivi karibuni.

Zitto alisema Mdee, Nassari, Kangi Lugola, Esther Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila walihudhuria Tamasha la Vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na Mratibu wa kundi hilo, Mwasiti Almasi na siyo kwa mwaliko wake.

Aliwataja wabunge wengine aliosema walialikwa kwenye hafla hiyo lakini hawakutokea, kuwa ni Joseph Mbilinyi, David Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. “Wabunge hawa hawakualikwa na mimi (Zitto), bali nilisaidia 'logistics' tu. Lengo la kushauriana na Vijana wa Kigoma All Stars kuwaalika wabunge kutoka vyama mbalimbali lilikuwa ni kuonyesha umoja na mshikamano wa nchi bila kujali vyama vya siasa,” alisema.

Zitto alisema tamasha hilo lilikuwa la muziki na halikuhusika kabisa na siasa. “Ni bahati mbaya sana kuwa kuna matamshi ya kisiasa yalitamkwa katika shughuli ile.”

“Waheshimiwa wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola. “Hotuba za wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na video hizo zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha lile la kihistori. “Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini walisema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema walioyasema Kigoma.

Nisingependa kuhusishwa kwa njia yeyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndiyo utasimama,” alisema. Zitto alionya “Suala la urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili kuhusu nchi yetu.

Taharuki ambazo watu wanazipata pindi masuala ya urais yanapotajwa, zinashangaza sana.” Zitto aliendelea kueleza kuwa chama chake Chadema hakijatangaza mchakato wa kupata mgombea urais na kitafanya hivi wakati mwafaka hivyo hakuna haja kugombana kwa hoja za urais sasa.

Kauli ya Mdee Alipotakiwa kuzungumzia mjadala huo jana, Mdee alikiri kuhudhuria hafla hiyo na kutoa maneno yaliyomliza Zitto lakini akasema hii ilitokana na historia yake kwenye siasa. “Maneno yangu hayakuwa na tatizo, shida ilikuwa ni context.

Ni kweli Zitto alilia kwa mimi kueleza namna alivyonilea kisiasa tangu nikiwa bado shule. Tatizo langu ni context tu.” Awali, Filikunjombe alipozungumza na gazeti hili kuhusu halfa hiyo alihoji: “Kwani tatizo ni nini? Hapa kuna habari ndugu… kuwa sehemu ya Tanzania kwa nini Kigoma isitoe rais?”

No comments:

Post a Comment

Thank you for visiting our website

Wazoefu Computer Technology

Search This Blog

Please Share This

Thanks for Like and Tweet